1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiZimbabwe

Zimbabwe yaanza kutumia sarafu yake mpya ya ZiG

2 Mei 2024

Zimbabwe imeanza wiki hii kutumia sarafu yake mpya inayofahamika kama ZiG na kuachana na sarafu ya zamani, katika jaribio lake la hivi punde la kutatua mzozo wa kifedha.

https://p.dw.com/p/4fQOH
Harare, Zimbabwe | Gavana wa Benki Kuu ya Zimbabwe John Mangudya
Gavana wa Benki Kuu ya Zimbabwe John Mangudya Picha: JEKESAI NJIKIZANA/AFP

Jumanne wiki hii, Zimbabwe ilianza kusambaza sarafu yake mpya ya ZiG ambayo imechukua nafasi ya sarafu ya zamani iliyofahamika kama "dola ya Zimbabwe" ambayo ilishuhudia kupoteza thamani yake na mara nyingi kukataliwa kabisa na raia wa nchi hiyo.

Sarafu ya ZiG yenye maana kwa kiingereza "Dhahabu ya Zimbabwe", ilianzishwa kielektroniki mapema mwezi Aprili, lakini sasa watu wanaweza kutumia noti na vichele vya sarafu hiyo mpya.

Soma pia:Mnangagwa asamehe wafungwa 4,000

Hili ni jaribio la hivi punde la nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kujaribu kumaliza mgogoro wa kifedha ambao ni sehemu ya matatizo yake lukuki ya kiuchumi.

Hapo awali serikali ilitoa mapendekezo mbalimbali ambayo yangelikuwa mbadala wa dola ya Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na kujaribu kutumia sarafu za kidijitali au kuanzisha sarafu za dhahabu ili kupunguza mfumuko wa bei.

Sarafu ya ZiG kueleta tofauti kwenye uchumi wa nchi?

Tangu sarafu ya ZiG ambayo thamani yake inatokana na akiba ya dhahabu ya nchi hiyo kuzinduliwa kielektroniki tarehe 5 Aprili, inaonekana pia kuelekea katika mkondo wa kutoaminika huku baadhi ya idara za serikali zikikataa kabisa kuitumia.

Zimbabwe | Mjasiriamali na fundi wa kushona mavazi akiwa katika majukumu yake
Mjasiriamali na fundi wa kushona mavazi akiwa katika majukumu yakePicha: DW

Lakini Baadhi ya raia wana matumaini makubwa na sarafu hii ya ZiG na kusema itapandisha thamani ya fedha ya nchi hiyo.

"Nina uhakika shughuli zote zitakuwa rahisi kwa kuwa tunayo ZiG, tunaweza kufanya manunuzi kwa urahisi. Ilikuwa ngumu, hasa katika mabasi ya abiria ambapo watu walikuwa wakigombana ili kupata chenji." Mmoja wa raia alisema.

Soma pia:Zimbabwe yatangaza ukame kuwa janga la kitaifa

ZiG ni sarafu ya sita kutumiwa nchini Zimbabwe tangu sarafu ya zamani ya nchi hiyo kushuhudia anguko lake mnamo mwaka 2009 huku kukiwa na mfumuko mkubwa wa bei kuwahi kushuhudiwa duniani ambao ulifikia viwango vya asilimia bilioni 5.

Hali hiyo ilifuatiwa na mfululizo wa matatizo ya kiuchumi na kifedha ambapo dola ya Marekani iliruhusiwa kutumiwa kama zabuni halali, kisha ikapigwa marufuku na baadaye kuruhusiwa tena.

Nafasi ya dola ya Marekani dhidi ya ZiG

Wakati sarafu mpya ya ZiG ikitangazwa kuwa zabuni halali nchini Zimbabwe, bado raia wa nchi hiyo wanaonekana kuwa na mashaka na kuendelea kuiamini dola ya Marekani ambayo wanasema inatoa hakikisho zaidi kwa mali zao.

Baadhi ya raia wa Zimbabwe wanasema hawaelewi vyema thamani halisi ya sarafu hiyo mpya ya ZiG.

"Naogopa kwamba watu wengine watanitapeli kwa sababu sielewi thamani ya sarafu hii. Tunahitaji mtu anayeweza kutufundisha, niliwauliza hata benki lakini na wao pia wakasema hawajui." Alisema Susan Chikumene

Mbali na hayo, kumekuwa na mkanganyiko nchini Zimbabwe kuhusu matumizi rasmi ya sarafu hii ya ZiG.

Kilimo cha ngano Zimbabwe

Soma pia:Asilimia 44 ya mazao ya mahindi nchini Malawi yameathirika na ukame

Serikali mjini Harare imewaruhusu baadhi ya wafanyabiashara, kama wale wanaomiliki vituo vya mafuta na mamlaka ya kutoa pasipoti za kusafiria, kukataa kupokea sarafu hiyo ya ZiG na badala yake wakaruhusiwa kuchukua pekee dola za Marekani.

Wakati huo huo, wamiliki wa biashara zingine wameamriwa kutumia pekee sarafu ya ZiG, na iwapo watakiuka agizo hilo basi watakabiliwa na hatua kali.

Serikali ya Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa imewakamata makumi ya wafanyabiashara wanaoendesha harakati haramu wakituhumiwa kujaribu kuihujumu sarafu hiyo mpya.